MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeamuru mfanyabiashara Yusuf Manji ambaye alikuwa kizuizini chini ya Idara ya Uha...
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es
Salaam imeamuru mfanyabiashara Yusuf Manji ambaye alikuwa kizuizini
chini ya Idara ya Uhamiaji, kuachiwa huru chini ya dhamana aliyopewa
kwenye kesi namba 63 ya kutumia dawa za kulevya iliyopo Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu.
Manji aliondoka mahakamani hapo na kuingia katika hoteli moja maarufu jijini Dar es Salaam akiwa na mlinzi wake.
Hatua hiyo imekuja baada ya jopo la
mawakili wa mdai, Alex Mgongolwa, Alex Musumbushi na Jeremiah Ntobesya
kuieleza mahakama kuwa mteja wao anashikiliwa na polisi kwa siku 30.
Mgongolwa alidai Manji akiwa Hospitali
ya Aga Khan walikuwepo askari sita waliokuwa wanamlinda na kwamba hata
jana aliletwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi.
Pia alidai katika kiapo cha Ofisa wa
Uhamiaji, Arnold Munuo amekiri kwamba alimchukulia maelezo Manji, hivyo
ni kweli kwamba wanamshikilia.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Osward
Tibabyenko alidai kuwa maofisa hao wa polisi hawamshikilii Manji, hatua
ambayo Jaji Ama Munisi alitaka kujua ukweli kuhusu suala hilo.
Jaji Munisi aliutaka upande wa mdai kuleta vielelezo vya kuthibitisha kama kweli mshitakiwa alikuwa kizuizini.
Aidha, aliamuru Manji kuwa huru kwa
dhamana aliyoipata katika kesi namba 63 ya mwaka huu ambayo ni ya
kutumia dawa za kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Pia alisema maombi hayo yatasikilizwa
Machi 27, mwaka huu na kiapo kuhusu kuthibitisha kama kweli Manji
aliwekwa kizuizini itapelekwa Machi 24, mwaka huu.
Mgongolwa alidai watawasilisha
mahakamani hapo hati ya kiapo ya wafanyakazi wa Aga Khan hospitali na
majina ya askari waliokuwa wakimshikilia Manji ili kuthibitisha suala
hilo.
Katika kesi hiyo wajibu maombi hayo ni
Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam.
Katika maombi hayo, yaliyopelekwa
mahakamani hapo na Wakili Hudson Ndusyepo, alieleza kushangazwa na
kitendo cha mteja wake kuwekwa chini ya ulinzi na Idara ya Uhamiaji
akiwa Hospitali ya Aga Khan ambapo anashikiliwa isivyo halali, hivyo
wanaiomba mahakama kumwachia huru.
Manji alikuwa chini ya ulinzi baada ya
kuachiwa kwa dhamana, Februari 20, mwaka huu alipopelekwa Ofisi ya
Uhamiaji Mkoa na kuhojiwa kwa madai ya kuingiza wageni nchini kinyume
cha sheria.
Wakili wa Manji, Ndusyepo alifungua kesi
ya maombi hayo, akitaka mahakama iagize maofisa uhamiaji na polisi
kumfikisha mahakamani ili iamue uhalali wa kushikiliwa kwake na kuagiza
aachiwe.
Katika hati ya maombi hayo, Ndusyepo
anadai kuwa alimtembelea mteja wake Hospitali ya Aga Khan, Februari 17,
mwaka huu na kukuta maofisa wa uhamiaji wakimsubiri mteja wake wampeleke
kwa ofisa uhamiaji mkoa kwa mahojiano dhidi ya tuhuma siyo raia wa
Tanzania.
Kwa mujibu wa Ndusyepo, Manji amedai
kuwa alitoa maelezo kwa maofisa uhamiaji na alirudishwa Aga Khan ambako
yupo chini ya ulinzi hadi sasa.
Katika kesi inayomkabili Kisutu, Manji
ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu alifikishwa mahakamani hapo
kwa mara ya kwanza Februari 16, mwaka huu akidaiwa kuwa kati ya Februari
6 na 9, mwaka huu, katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa
za kulevya aina ya heroin, ambayo aliachiwa kwa dhamana ya Sh milioni
10.
COMMENTS